DAKIKA 90 ZA SINTOFAHAMU NCHINI UINGEREZA

Ni dakika 90 za sintofahamu kwenye viwanja mbalimbali nchini Uingereza. Na hii ni kutokana na fomu pamoja uwezo wa timu hizo zinazomenyana wikiendi hii kushabihiana ukiachilia mbali usajili uliofanywa na baadhi ya timu hizo.

14:30 EAT - West Ham United vs Tottenham 
Mapema kabisa vijana wa London watamenyan aikiwa ni West Ham United watawakaribisha Tottenham kwenye dimba la London Stadium. West Ham United imekuwa ikihangaikakutafuta matokeo mazuri tangu kuanza kwa msimu wa 2017/2018 na kufanikiwa junyakua pointi 4 tu kwenye mechi 5. Timu hiyo imefunga magoli 4 na kuruhusu 10 nyavuni mwake. Hiyo ni ishara ya safu mbovu ya ulinzi na safu butu ya aidha ushambuliaji au kiungo. Kwa kuwa kwa mchezaji mmoja mmoja wana uwezo basi tutegemee mabadiliko siku baada ya siku. Na vipi hiyo siku baada ya siku ikianza leo?
Kwa upande wa Tottenham, ni timu bora iliyojiimarisha tangu msimu uliopita japokuwa hawakuanza msimu kama ilivyotegemewa na wengi ukichukulia kwamba hawajauza wachezaji wao bora isipokuwa beki wa kulia Kyle Walker aliyetimkia Manchester City. Kuondoka kwa Walker siyo tatizo kwa Spurs ukizingatia kwamba wameruhusu goli 3 kwenye mechi 5, hii ni ishara ya safu nzuri ya ulinzi. Leo itakuwa ni vita ya mshambuliaji hatari, Harry Kane na safu dhaifu ya ulinzzi ya West Ham United. 

17:00 EAT - Burnley vs Huddersfield Town 
Huu utakuwa mtanange wa wabishi wa ligi. Wote wana pointi 8 kila mmoja, wakiwa wameshinda michezo miwili, sare mbili na kupoteza mmoja kila mmoja. 

17:00 EAT - Everton vs Bournemouth
Wote wakiwa wanashika mkia kwenye msimamo wa Ligi. Ni vita ya kujitoa kutoka kwenye shimo la moto ili kuepuka kudidimizwa zaidi. Wakiwa wamefanikiwa kushinda mchezo mmoja kwenye mechi tano za ligi, Everton na Bournemouth ni miongoni mwa timu zilizoonyesha udhaifu kwenye safu zote za ulinzi na ushambuliaji. Je ni nani atarudisha makali yake na kurudisha hofu kwa wapinzani? 

17:00 EAT - Southampton vs Manchester United
St. Mary's Stadium patachimbika leo. Manchester United inayoongozwa na Jose Mourinho itahitaji kuendeleza ubabe wake dhidi ya timu za England. Je, Southampton itaweza kuwasimamisha? Timu hiyo yenye mshambuliaji hatari wa paundi milioni 75, Romelo Lukaku na kiungo machachari na mchawi wa mpira Henrik Mkhtaryan ni moja ya timu zenye safu hatari ya ushambuliaji na safu kali ya ulinzi kwenye ligi kuu ya Uingereza na hata kwenye ligi tano bora za barani Ulaya. Ikumbukwe mara ya mwisho Manchester United kutoka na ushindi kwenye dimba la St. Mary's ni Septemba 2015. 

17:00 EAT - Manchester City vs Crystal Palace 
Timu iliyofunga goli 16 na kuruhusu goli 2 kwenye michezo mitano inamenyana na timu iliyoruhusu goli 8 na kutofunga hata moja kwenye michezo mitano, hali iliyopelekea kufukuzwa kwa kocha De Boer. Crystal Palace atapata goli lake la kwanza la msimu au ataendeleza ukame? Hii itatokana na nguvu kazi itakayowekwa na wachezaji pamoja na mbinu za kocha mpya. Mara ya mwisho Crystal Palace kuifunga Manchester City ni April 2015.

17:00 EAT - Stoke City vs Chelsea
Ndani ya dimba gumu la Brittania Stadium, Stoke City wataikaribisha Chelsea ya London, Stoke City wakiwa na kumbukumbu ya kuikaribisha Arsenal ya London na kuonyuka 1-0. Stoke City ni timu inayosifika kwa kuwa na safu nzuri ya ulinzi ukijumlisha na satili yake ya mpira wa 'Counter-Attack'. Ni miongoni mwa timu zinazoumbua timu kubwa nchini Uingereza. Stoke City pia ndio timu pekee iliyoizuia Manchester United kwa kuilazimisha sare ya 2-2. Usajili wa Choupo-Moting na Jese Rodriguez umeongeza chachu ya ushambuliaji ya timu hiyo. Kwa upande wa Chelsea, ni timu iliyoimarika kila idara. Ina goli kipa wa kiwango cha dunia, safu kali ya ulinzi, kiungo na washambuliaji hatari wakiongozwa na Alvaro Morata aliyesajiliwa kutoka Real Madrid kwenye dirisha la majira ya joto.

17:00 EAT - Swansea City vs Watford 
Tusitegemee kuona magoli mengi kwenye mechi hii. Timu hizi hucheza kwa nidhamu ya hali ya juu zinapocheza pamoja. Ni timu zinazojilinda zaidi na kushambuliana kwa zamu. Nani ataibuka mbabe leo?

19:30 EAT - Leicester City vs Liverpool
Mara ya mwisho wamekutana kwenye Kombe la Ligi siku chache zilizopita. Leicester City wamefunga goli 7 na kuruhusu goli 9 kwenye mechi 5. Liverpool wamefunga goli 9 na kuruhusu 9 kwenye mechi 5. Tutegemee magoli mengi kwenye mechi hii.
Utakuwa ni usiku mzuri kwa wapenda soka kwani ni usiku wa mabao.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

KOCHA TAIFA STARS ATANGAZA KIKOSI CHA MAANGAMIZI